December 9, 2011

UNEGRO

Dhana ya Unegro kwa kifupi inahusiana moja kwa moja na rangi nyeusi. Neno “Unegro” mpaka kufikia lugha ya Kiswahili limepitia lugha kadhaa. Neno la asili ni “niger” ambalo ni neno la Kilatini likimaanisha rangi nyeusi. Baadaye neno hili likakopwa katika lugha ya Kifaransa na kuwa “nègre”. Ingawa neno hili linamaanisha rangi nyeusi, lilitumika kwa kumaanisha watu weusi. Kwa hiyo ni neno ambalo lilibeba dhana ya tusi au kejeli kwa mtu mweusi. Kwa hiyo neno lenyewe katika lugha ya Kifaransa ni Négrité ambalo lilitafsiriwa katika Kiingereza kama “negritude” likibeba dhana iliyoonekana ni mtazamo au mkondo wa falsafa ambao kwa lugha ya Kiswahili tunauita “unegro”. Kama tulivyoona hapo juu, asili ya mtazamo au mkondo huu wa kifalsafa unatokea katika lugha ya Kifaransa na kwa hakika waanzilishi wa dhana hii ni watu weusi waliotawaliwa na nchi ya Ufaransa.

Tofauti na wale waliotawaliwa na Waingereza kama vile akina Nyerere, Nkrumah, na Kaunda ambao mitazamo yao iliwasilishwa kwa njia ya vitabu vilivyofafanua dhana hizo, waanzilishi wa unegro walitumia sanaa ya fasihi. Kwa hiyo unegro ni harakati za kisiasa na kifasihi kwa sababu zilitumia fasihi kama chombo cha kuelezea fikra na mawazo yao ya mtu mweusi.

Pamoja na ukweli kuwa dhana ya unegro haina chembechembe za kibaguzi au hisia zozote za unyanyasaji katika lugha ya Kiswahili, neno “négrité” katika lugha ya Kifaransa kwa wakati huo lilionyesha hisia hizo za kubaguliwa, kutengwa na kunyanyaswa. Kwa hiyo, mkondo huu wa mawazo ulianzishwa ili kupambana na unyanyasaji unaotokana na ubaguzi wa rangi, kupinga sera ya usimilishaji (assimilation policy) wa Kifaransa ambao ulilenga kumtenganisha Mwafrika na asili yake, yaani mila, desturi na lugha ama tuseme utamaduni kwa ujumla.

Tukumbuke kwamba mkondo huu wa mawazo sio uliozaa harakati za kutafuta utambuzi na urazini wa mtu mweusi, bali ni katika harakati za kujitambua ndipo mkondo huu wa mawazo uliibuka. Kama ilivyo kwa watu waliotawaliwa na Waingereza na Wamarekani wenye asili ya Kiafrika walioanzisha Umajumui wa Kiafrika (Pan Africanism), kwa upande wa makoloni ya Kifaransa ulianzishwa mkondo huu wa Unegro, ingawa dhana za msingi ni zilezile za kutafuta uhuru, utambuzi na mustakabali mpya wa mtu mweusi mwenye asili ya Afrika.

Waanzilishi wa mkondo harakati/itikadi/mkondo wa mawazo au falsafa ni Léopold Sédar Senghor (1906 - 2001), Aimé Césaire (1923-2008) na Leon Gontran Damas (1912- 1978). Mawazo makuu ya unegro tunayapata katika kazi mbalimbali za kifasihi kama vile Cahier d'un retour au pays natal kazi ambayo ilitafsiriwa katika Kiingereza na kuitwa Return to My Native Land ambayo tunaweza kuitafsiri kwa Kiswahili kama Kurejea Asili Yangu kazi iliyoandikwa na Aimé Césaire mwenyeji wan chi ya Martinique kisiwa mojawapo cha Karibiani. Kwa kifupi hii ni kazi ya kisanaa ambayo imeandikwa kishairi na kinathari ikielezea athari mbaya za utumwa na ukoloni. Aidha, Léopold Sédar Senghor, ambaye ni mwenyeji wa Senegali, alindika kazi mbalimbali za kishairi mojawapo ni Anthologie de la nouvelle poésie nègre et malgache (Diwani ya Mashairi Mapya ya Wanegro na Wamalagasi, 1948). Na Leon Gontran Damas mwenyeji wa Guyana, aliandika kazi mbalimbali ikiwemo ile ya Black Label (Utambulisho wa Mtu Mweusi, 1956). Hawa wasanii na wanafalsafa ya unegro walieleza mawazo yao mbalimbali katika kazi zao za fasihi. Waliwahi pia kuanzisha jarida L'étudiant noir (Mwanafunzi Mweusi) ambalo lililenga kuimarisha umoja wa wanafunzi weusi bila kujali utaifa wao, yaani wajione wote kama wamoja.

Kwa kifupi, tunaweza kusema kuwa unegro ni harakati za kudai utambulisho wa mtu mweusi ambaye asili yake ilikuwa inapotezwa kwa makusudi, kupinga unyanyasaji unaofanywa na Ufaransa dhidi ya watu weusi wa maeneo mbalimbali, na kupinga usilimishaji uliowataka watu weusi waachane na tamaduni zao za kishenzi zisizokuwa za kistaarabu badala yake wachukue tamaduni za Kifaransa zilizostaarabika.

No comments:

Post a Comment